Programu ya Imarisha Uchumi na Samia (IMASA) ni Programu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, ambayo imejielekeza kwa Wanawake, Vijana, Wazee na wenye Ulemavu. Programu hii inalenga kuboresha shughuli za kiuchumi za wananchi wa Tanzania kupitia Ofisi za wakuu wa Mikoa. Programu hii imeasisiwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia programu hii amedhamiria kuwawezesha wananchi kiuchumi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Katika kutekeleza azma hii Serikali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje itahakikisha mafanikio yanafikiwa katika kuwawezesha wananchi.
NEEC inaratibu na kusimamia utekelezaji wa Programu hii kwa kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Manispaa, Halmashauri za Majiji, Manispaa, Halmashauri za Miji, Wilaya na Wadau wa Maendeleo katika sekta husika. Programu hii imepangwa kutekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ni kufanya mapitio ya hali halisi na kukusanya takwimu na awamu ya pili ni kubuni programu za uwezeshaji kwa kila Mkoa na kuanza utekelezaji.
Programu hii ambayo inatekelezwa katika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar imeanza utekelezaji wa awamu ya kwanza hadi kufikia Desemba, 2024 wananchi 86,596 na vikundi 4,215 wamefikiwa na kusajiliwa kupitia dodoso la kidijitali (e-Dodoso), ambapo wananchi 85,361 ni kutoka mikoa (26) ya Tanzania bara na 1,235 kutoka mikoa (5) ya Zanzibar na vikundi 4,077 kwa Tanzania bara na vikundi 138 kwa Zanzibar.
Madhumuni ya Programu
Programu hii inalenga kuwawezesha wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar na ina madhumuni yafuatayo:
- Kupata takwimu za wananchi waliopo kwenye maeneo husika na shughuli zao za kiuchumi katika maeneo hayo.
- Kupata takwimu za Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi
- Kupata vipaumbele vya kiuchumi kwa kushirikiana na viongozi wa Mikoa na Wilaya ambavyo vitafikia wananchi wengi.
- Kubuni na kutekeleza programu ya kuwawezesha wananchi kwenye mikoa na maeneo yao.
- Kuunganisha program zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mpango huu.
Muda wa Utekelezaji
IMASA ni mradi endelevu unaolenga kutatua changamoto za muda mrefu za kiuchumi zinazowahusu wanawake, wazee, vijana na watu wenye ulemavu nchini. Mradi huu utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano 2025-2030. Aidha utekelezaji wake ni wa kipindi cha mwaka mmoja mmoja kuanzia mwaka huu wa 2025 na hivyo maombi ya fedha za utekelezaji kuwasilishwa katika kila kipindi cha mwaka wa fedha husika.
Hitimisho
Imarisha uchumi na Samia, ni mradi uliosheheni afua zinazoakisi mahitaji yaliyoibuliwa na wananchi katika Mikoa mbalimbali katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi ambapo viongozi, sambamba na wananchi wao waliweza kujitokea na kuweka mitizamo yao juu ya maeneo ya msingi yanayoweza kufanyiwa kazi na kutatua changamoto zinazoweza kuchochea maendeleo ya Mkoa husika. Katika kuchambua changamoto husika kila Mkoa, uliweza kubainisha uwepo kwa changamoto nyingi zinazoshabihiana na maeneo mbalimbali ambayo ni vipaumile vya Taifa na hivyo kutajwa kwenye mikakati mbalimbali ya kitaifa ikiwemo, Mpango wa maendeleo ya Taifa na Ilani ya Uchaguzi. Dhamira thabiti ya mradi ni kwenda kutatua changamoto ya umasikini wa kipato kwa Watanzania.