Programu ya Mpango wa Kuendeleza Viwanda Vidogo na vya Kati

SANVN Viwanda Scheme ni Programu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kutatua changamoto ya upatikani wa ujuzi, masoko, teknolojia na mitaji katika miradi ya viwanda vidogo na vya kati katika eneo la kuongeza mnyororo wa thamani viwandani.  Walengwa wa Mpango huu ni Wajasiriamali wadogo na wa kati wenye viwanda wanaojishughulisha katika kuzalisha bidhaa ili kuongeza mnyororo wa thamani. Programu hii inaratibiwa na taasisi tano (05) ambazo ni SIDO, AZANIA BANK, NSSF, VETA na NEEC. Makubaliano ya utekelezaji baina ya taasisi hizi yalitiwa saini tarehe 21 Februari, 2020 na Mpango ulizinduliwa rasmi tarehe 10 Julai, 2020 Mkoani Dodoma. Aidha, baada ya kuzinduliwa mpango huu mikopo ilianza rasmi kutolewa mwezi septemba, 2020.

VIGEZO VYA KUNUFAIKA NA PROGRAMU YA SANVN VIWANDA SCHEME

SANVN Viwanda Scheme inatoa mikopo ya kuanzia shilingi Milioni 8 - Milioni 50 kwa viwanda vidogo na Shilingi Milioni 51 - Milioni 500 kwa viwanda vya kati. Aidha, mikopo hii imegawanyika katika makundi mawili ambayo ni mikopo ya uwekezaji na mikopo ya uendeshaji wa miradi.

MIKOPO YA UWEKEZAJI

Mikopo ya uwekezaji ni mikopo itolewayo kwa ajili ya ununuzi wa mashine/mitambo ili kuanzisha/kuendeleza viwanda vidogo au vya kati (SMEs). Muda wa urejeshaji ni kati ya mwaka 1-7; Kiasi cha mkopo ni kati ya shilingi milioni nane (8 mil) na milioni mia tano (500 mil);

MIKOPO YA UENDESHAJI

Mikopo chini ya kundi hili hutolewa kwa lengo la kuwezesha shughuli za kiutendaji za kila siku mfano ununuzi wa malighafi, vifungashio, matangazo na gharama zingine za uendeshaji. Muda wa urejeshaji ni kati ya mwaka 1-3; Kiasi cha mkopo ni kati ya Shilingi milioni nane (8 mil) na milioni mia tano (500 mil);

VIGEZO NA MASHARTI YA UJUMLA

  1. Mwombaji awe na dhamana yenye thamani ya 125% ya kiwango cha mkopo. Kwa mkopo wa mashine/mitambo ya uzalishajii, mkopaji atalipia 20% ya gharama ya mashine/mitambo na mkopo utalipa 80% na mashine/mtambo husika utakuwa dhamana ya mkopo; na
  2. Mwombaji atatakiwa kutoa uthibitisho wa mkataba wa upangaji au umiliki wa eneo la mradi;
  3. Riba ya 13% itatozwa kwa mwaka (riba itatozwa kwenye salio la mkopo);
  4. Kwa waombaji wa Vikundi: kikundi ni lazima kiwe cha watu 5-10 na kitatakiwa kuwa na barua ya utambulisho toka taasisi inayowasimamia; na
  5. Bima ya mkopo ni asilimia mbili (02) ya kiwango cha mkopo kilichoidhinishwa na itatozwa kwa mara moja;
  6. Mwombaji lazima awe na umri usiopungua miaka 18 na awe raia wa Tanzania; Pia Mikopo ya vikundi hutolewa kwa vikundi vyenye watu kati ya 5 na 15 vilivyoundwa na SIDO au VETA kupitia Program zao mbalimbali.
  7. Mradi lazima uwe umesajiliwa kisheria, umefanyiwa upembuzi yakinifu wa kifedha na unakubalika kijamii
  8. Mradi ni lazima uwe wa uzalishaji bidhaa (kiwanda) na kuendeshwa kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja (01);
  9. Mwombaji awe anakusudia kuanzisha kiwanda kwa sharti la kuwa na vyanzo vingine vya mapato kupitia ajira, biashara, kilimo au shughuli nyingine inayoweza kuonesha uwezo wa kurejesha mkopo anaohitaji;
  10. Mwombaji lazima awe mnufaika wa huduma za SIDO au VETA na atatakiwa kutoa uthibitisho wa huduma aliyopatiwa SIDO au VETA; Na awe mwanachama wa NSSF au awe tayari kujiunga uanachama;

MATOKEO YA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA SANVN VIWANDA SCHEME

Toka programu ianzishwe Julai, 2020 hadi kufika Desemba, 2024, maombi ya mikopo ipatayo 324 yenye thamani ya shilingi bilioni 88.54 ilipokelewa na SIDO na kuwasilishwa benki ya Azania. Na jumla ya miradi midogo na ya Kati ipatayo themanini na tano (85) imenufaika na mikopo kutokana na programu hii katika mikoa 13 ambayo ni Mwanza, Arusha, Dar Es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Geita, Songwe, Dodoma, Pwani, Singida, Rukwa, Njombe na Shinyanga.

Programu imewezesha upatikanaji wa bidhaa ambazo ililazimu kuagiza kutoka nje ya nchi, kwa mfano imewezesha viwanda mbalimbali kama ECO Consumer wanaozalisha kemikali za viwandani na vipodozi na Amiron medical equipments watengenezaji wa vifaa tiba waliopo mkoa wa Pwani na Bongo toothpick watengenezaji wa bidhaa za kimbaka (toothpicks) waliopo mkoa wa Dar Es Salaam. Viwanda hivi vimewezesha upatikanaji wa bidhaa bora kwa gharama nafuu nchini.

Ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zilizozalishwa kutokana na utekelezaji wa programu hii tangu ianzishwe hadi kufikia Desemba, 2024 zilikuwa 14,956 (wanawake 8,309 na wanaume 6,647). Hii ilitokana na hamasa ya wanufaika kukidhi vigezo ili kutumia fursa za uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo na vya kati kupitia Mpango katika shughuli za kiuchumi.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo